RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI DKT. HUSSEIN MWINYI AMEKUTANA NA ZEC IKULU
- babalaoshaibu
- Nov 10, 2020
- 1 min read
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa shukurani na pongezi kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kwa kufanikisha vyema Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2020.
Shukurani hizo na pongezi amezitoa leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), wakiwemo Makamishna wa Tume hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud pamoja na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Thabit Idarous Faina.
Katika maelezo yake Rais Dkt. Hussein Mwinyi aliueleza uongozi huo wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) kwamba ameona haja ya kuwaita viongozi hao baada ya kukamilika mchakato wa uchaguzi kwa azma ya kuwashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya.
Alieleza kuwa Tume hiyo imetekeleza vyema kazi zake hivyo, kuna kila sababu ya kuishukuru na kuipongeza kwa mafanikio hayo makubwa yaliopatikana licha ya baadhi ya changamoto zilizojitokea katika kipindi hicho cha uchaguzi.
Hivyo, Rais Dkt. Hussein aliwaahidi viongozi hao kuwa ataendelea kutoa ushirikiano wake kwao na kusisitiza kwamba milango yake iko wazi akimaanisha kwamba yuko tayari kushirikiana nao na kuwasikiliza wakati wowote.
Wakati huo huo, Rais Dkt. Hussein Mwinyi alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Zanzibar na kuvipongeza vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kipindi chote cha kabla, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Comments