YALIYOJIRI WAKATI WA UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA KIWANDA NA UFUNGUZI WA CHUO CHA POLISI
- mwanzos12
- Feb 26, 2021
- 2 min read
Aliyosema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
Nitumie fursa hii kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa za kizalendo wanazozifanya kwa kusimamia usalama, amani na utulivu wa nchi yetu, Asanteni sana. IGP fikisha shukrani hizi kwa askari wote, uhalifu umepungua sana hasa ule wa kutumia silaha.
Nimeambiwa jengo lenye nyumba za askari halijaanza kutumika, msisubiri, ni vyema sasa askari waanze kulitumia jengo hilo, watoke kwenye 'magofu,' mimi napenda askari wangu wakae mahali pazuri.
Chuo hiki kina historia ya kipekee katika nchi yetu, kilianza tangu mwaka 1958, maofisa wengi wa jeshi na viongozi wengine walipata mafunzo hapa, kwa heshima ya chuo hiki nitawaletea bil 1 ili mjenge majengo mengine, mmenifurahisha sana
Niliona mna mpango wa kujenga hospitali hapa, nimefikiria nikaona hakuna ubaya tukijenga vituo vya afya katika taasisi za majeshi ili askari na familia zao wawe wanatibiwa hapa pamoja na wananchi wanaozunguka maeneo haya, hivyo nitawaletea shilingi milioni 500 ili hospitali kubwa ijengwe hapa.
Nakuagiza Waziri na viongozi wengine wa Wizara ya Mambo ya ndani kwenda Wizara ya Fedha kufuatilia malipo ya askari wastaafu walipwe ndani ya wiki moja ili wafurahie kustaafu kwao kwani wamelitumikia Taifa kwa Uzalendo
Nakuagiza IGP uweke utaratibu wa kukaa vikao na askari wa vyeo vya chini ili kusikiliza kero zao, wakati mwingine wanashindwa kuzungumza kwa sababu ya taratibu za kipolisi, jua kuhusu posho zao na masuala yao yote, hii inasaidia
Nimefurahishwa na kazi mnazozifanya, hasa mpango wa kuanza kutengeneza sare kwa ajili ya askari wetu, ninaahidi kushirikiana nanyi katika kutatua changamoto zote zilizopo
Nawapongeza na kuwashukuru sana viongozi wa dini mlivyo na umoja katika kuliombea Taifa letu amani, nawashukuru jeshi la polisi kwa uchapakazi na umakini katika kuimarisha amani ya Tanzania katika kupambana na maadui mbalimbali, endeleeni hivyo na Mungu awabariki sana, niko pamoja nanyi na nitaendelea kutatua changamoto zenu.
Aliyosema Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. George Simbachawene
Nakupongeza Mhe. Rais kwa sababu ya msimamo wako na uamuzi wa kutekeleza miradi kwa kukataa mifumo ya kimagharibi na kufuata mfumo wa nguvu kazi (Force Account) ndio maana miradi inayotekelezwa na takribani taasisi zote za umma zinakamilika katika takribani nusu ya gharama zinazokuwa zimekadiriwa awali tofauti na hali ilivyokuwa hapo zamani kabla ya kuanza kutumia mfumo huu
Aliyosema IGP Simon Sirro, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania
Majengo haya yanayojumuisha bweni lenye ghorofa 4, jengo la utawala, ofisi za walimu na madarasa yamekamilika kwa gharama ya shilingi milioni 799.6 badala ya gharama zilizokariliwa awali shilingi bil. 1.5 hivyo kuokoa fedha za Serikali takribani shilingi milioni 760. Chuo kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 625 badala ya 440 ikiwa ni nyongeza ya asilimia 42.04 ya uwezo wake
Ujenzi wa kiwanda cha kisasa umegharimu shilingi milioni 666.4 badala ya bil 1.4 hivyo kuokoa fedha za Serikali shilingi milioni 700 na kitakamilika mwezi Machi, 2021.
Hali ya usalama nchini kwetu ni shwari japo yapo baadhi ya matukio machache ya uhalifu, ila wahalifu wote wanakamatwa na sheria inachukua mkondo wake, kwa hiyo kwa ujumla tuko vizuri.
Kiujumla tumepunguza uhalifu kwa asilimia 13.5, hii ni takwimu ya mwaka 2019 na 2020 inayojumuisha makosa mbalimbali ikiwemo ya kuwania mali, makosa ya kutumia silaha, Watanzania watuelewe kwamba awamu hii sio ya kujiingiza kwenye uhalifu, tutawashughulikia

















Comments