YALIYOJIRI WAKATI RAIS MAGUFULI AKIONGOZA KUUAGA MWILI WA KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI, KIJAZI
- mwanzos12
- Feb 19, 2021
- 2 min read
Updated: Feb 20, 2021
Aliyoyasema Rais Dkt. John Pombe Magufuli
"Natoa pole kwa watanzania kwa kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John William Kijazi".
"Siku moja nilipozungumza na Maalim Seif nilimuona ni mtu tofauti sana na jinsi picha yake ilivyokuwa imejengeka kwa sababu mazungumzo yetu yalikuwa mazuri na akanieleza kuwa hakushiriki kwenye uchaguzi wa pili (2015) lakini akasema "nakuhakikishia kuwa Zanzibar itakuwa salama, sitahamasisha fujo yoyote na miaka yote mitano aliyechaguliwa ataendelea vizuri kutawala", na hayo aliyafanya".
"Ninawaomba Watanzania, matatizo yoyote yanayotokea yatufanye tuwe wamoja zaidi kwani hofu ni mbaya, unapoona kuna kitu unashindwa kukitatua, mwambie Mungu kwa sababu yeye ndio muweza. Lakini tumefikia mahali tunatishana sana".
"Magonjwa yapo na yataendelea kuwepo, wala hayakuanzia hapa! Zipo nchi ambazo zimepoteza watu wake wengi. Sisi Tanzania Mungu ametusaidia katika kipindi cha ugonjwa mwaka uliopita hivyo tuendelee kusimama kwa kuchukua tahadhari na kumtanguliza Mungu".
"Inawezekena hili ni jaribu lingine lakini tukisimama na Mungu tutashinda, tusitishane na kuogopeshana kwa sababu tutashindwa kufika. Inawezekana kuna mahali tumemkosea Mungu au tunapata jaribu lakini ninatoa wito kuwa tusimame na Mungu".
"Ninawaomba Watanzania, kama kuna mahali tumetetereka tuendelee kumuomba Mungu na kufunga kuanzia leo, kesho na keshokutwa, viongozi wa dini endeleeni kuhimiza maombi, tutashinda. Kamwe Mungu hawezi kuliacha Taifa hili".
Waliyoyasema viongozi wengine
"Kiongozi huyu amefanya mambo makubwa ndani ya Serikali, sisi kama watumishi wa umma tunajua umakini, uhodari, uchapakazi na namna alivyokuwa na mapenzi mema kwa watumishi wenzake kwenye kutoa miongozo katika kusimamia shughuli mbalimbali za Serikali" - Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
"Sisi sote wajibu wetu sasa ni kuenzi mema na mazuri yote aliyoyafanya katika utumishi wake na katika uhai wake, tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kuiweka roho yake mahali pema peponi" - Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
"Kiongozi huyu ni kiongozi wa kuigwa kwani ametoa ushirikiano kwa kila mtu, hata katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alikuwa ni daraja zuri la kutuunganisha katika shughuli zetu za kiutendaji hivyo tunaendelea kumuombea" - Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
"Kwa niaba ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunatoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, familia na wananchi wote, tuko pamoja nanyi na tutaendelea kuwaombea katika kipindi chote hichi" -
Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson.
"Katika Sheria ya Utumishi wa Umma kuna sifa tatu ambazo Katibu Mkuu Kiongozi anatakiwa kuwa nazo ikiwemo Uongozi, Muelekeo na Taswira. Vyote hivyo alikuwa navyo, alikuwa makini hata kati
ka mambo madogo madogo ambayo wengine wanayadharau" - Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma.
"Tusisikitike sana bali tumkumbuke kiongozi wetu kwani alifanya kazi yake vizuri sana, mioyo yetu isiwe na huzuni kwasababu sifa zake ni nyingi zaidi kuliko kile kitone alichokiishi. Mungu atupe uwezo wa kustahimili katika hili" - Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma.