Tanzania Yaongoza Afrika Katika Viwango vya Ufanisi na Utawala Bora Duniani
- johnwengwi
- Sep 9
- 2 min read
Dar es salaam, Septemba 09, 2025
Chandler Good Government Index (CGGI) hupima ufanisi wa Serikali za nchi 120 duniani kwa kutumia nguzo saba kuu: uongozi na maono ya muda mrefu, sheria na sera madhubuti, taasisi imara, usimamizi wa fedha, soko lenye mvuto, nafasi na hadhi kimataifa, pamoja na uwezo wa kusaidia watu kupiga hatua kimaisha.
Tanzania imepanda hadi nafasi ya 78 duniani katika kipimo cha ufanisi wa Serikali kwa mwaka 2025 kupitia Chandler Good Government Index (CGGI), ikitoka nafasi ya 82 mwaka 2021. Mabadiliko haya yameifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza kwa mageuzi ya kiutawala barani Afrika katika kipindi hicho, kulingana na ripoti mpya ya CGGI.
Kupanda kwa hadhi hiyo kunachangiwa na uongozi wa kimkakati, mageuzi ya sera, na uwekezaji katika teknolojia ambayo imeimarisha utoaji wa huduma kwa umma. Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miradi kama e-Government na mpango wa Digital Tanzania, ambayo imeongeza uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma za kijamii.
Kupitishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kumeimarisha imani ya umma katika mifumo ya kidijitali, huku ikitoa mazingira salama kwa sekta binafsi na kwa mtu mmoja mmoja. Sera wazi na ushirikiano wa kimataifa pia vimechangia kuongezeka kwa imani ya wawekezaji. Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2024, uwekezaji wa ndani na wa kigeni uliongezeka kwa asilimia 21.6 hadi kufikia Dola za Kimarekani bilioni 6.56.
Ripoti ya CGGI pia imeonyesha maeneo ambayo Tanzania imepata alama za juu, ikiwa ni pamoja na uimara wa taasisi kwa asilimia 95, uwezo wa kusaidia watu kupiga hatua kimaisha kwa asilimia 86, heshima na ushawishi wa kimataifa kwa asilimia 83, sera na sheria madhubuti kwa asilimia 80, pamoja na soko endelevu na lenye mvuto kwa asilimia 77.
Katika ripoti hiyo, Tanzania na Rwanda ndizo nchi pekee za Afrika Mashariki zilizoonesha mafanikio makubwa ya kiutawala kati ya mwaka 2021 na 2025.
Mkurugenzi wa Ufuatiliaji wa Utendaji kutoka Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bi. Sakinah Mwinyimkuu, alisisitiza umuhimu wa kufuatilia utekelezaji wa sera, programu na miradi mbalimbali ili kuhakikisha zinatoa matokeo chanya. Alitaja pia falsafa ya “4Rs” ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa msingi wa muundo mpya wa utawala, falsafa inayojikita katika maridhiano (reconciliation), ustahimilivu (resilience), mageuzi (reforms), na ujenzi upya (rebuilding).
Aidha, Bi. Mwinyimkuu alieleza kuwa Tanzania ipo katika hatua ya mwisho ya kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayotarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2026. Dira hii inalenga kufuatilia kwa karibu viashiria muhimu vya maendeleo katika kipindi cha Mpango wa Tano wa Taifa wa Maendeleo, ikilenga maeneo yanayohitaji juhudi za ziada.
Kwa ujumla, matokeo ya CGGI yanaiweka Tanzania katika nafasi ya juu kikanda na kimataifa, yakionesha si tu uboreshaji wa viwango vya utawala, bali pia ukuaji wa uchumi unaoendelea na mazingira bora ya kuvutia wawekezaji.




Comments