Serikali yazindua Maeneo Malaalum ya kiuchumi na Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji Uwekezaji
- johnwengwi
- Aug 12
- 2 min read
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amezindua rasmi Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji Uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ), katika hafla iliyofanyika kwenye Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam leo Agosti 12,2025.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali, mabalozi, wadau wa sekta binafsi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali huku kukiwa na uzinduzi wa huduma ya TISEZA Whatsap Chatbot na SEZ e-handbook pamoja Maeneo Maalum ya Kiuchumi.
Prof. Mkumbo amesema kuwa uzinduzi huo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa dira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga uchumi wa viwanda na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji barani Afrika.
Pia amepongeza Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kwa mikakati ya kuunganisha SEZ na miradi mikubwa ya miundombinu kama Reli ya Kisasa (SGR), Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, bandari, barabara na viwanja vya ndege.
Aidha, amebainisha kuwa SEZ ni nyenzo muhimu duniani kwa kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira, kukuza mauzo ya nje, na kurahisisha uhamisho wa teknolojia.
"Tanzania ilianzisha Mamlaka ya EPZA mwaka 2006 kupitia Mpango wa Mini Tiger 2004–2020, na kutenga maeneo 34 ya SEZ pamoja na zaidi ya maeneo 200 ya Stand-Alone EPZ."
Hata hivyo, Waziri ametaja changamoto za kodi, gharama kubwa za upangishaji, na ukosefu wa mkakati wa kitaifa kama vikwazo vilivyochelewesha maendeleo ya SEZ.
Pia Prof. Kitila amesema kuwa kupitia TISEZA, Serikali imetambua maeneo matano ya kimkakati kwa uwekezaji ambayo ni Nala lililopo umbali wa kilomita 21kutoka Dodoma mjini na lenye ukubwa wa hekta 607 na linaviwanja 259.
Na eneo la Kwala SEZ lilipo mkoa wa Pwani, Buzwagi SEZ lililopo mkoani Shinyanga, Bagamoyo Eco Maritime City lililopo mkoa wa Pwani na upanuzi wa Benjamin William Mkapa SEZ (Dar es Salaam).
Amesema pia serikali imetoa vivutio vingi ikiwemo msamaha wa kodi ya mapato ya kampuni hadi miaka 10 kwa miradi inayokidhi vigezo, lengo likiwa kuwahamasisha wawekezaji wa ndani na nje.







Comments