Mhe. Samia Suluhu Hassan Aapishwa kuwa Rais wa Tanzania
- mwanzos12
- Mar 19, 2021
- 2 min read
Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameapishwa kuwa Rais wa Tanzania leo Tarehe 19/03/2021 katika hafla ndogo iliyofanyika katika Ikulu ya Magogoni Jijini Dar-es-Salaam na kuhudhuriwa na Marais wastaafu wa Tanzania na Zanzibar.
Mara baada ya Mama Samia Kuapishwa kuwa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania alipigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride maalumu kwa mara ya kwanza akiwa Ndiye amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Mama Samia mwenye umri wa miaka 61, amekuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huu nchini Tanzania. Ameshika wadhifa huo kufuatia kifo cha Rais John Pombe Magufuli kilichotokea Jumatano, Machi 17, 2021.
Rais Samia atashikilia wadhifa huo kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa Urais mpaka 2025, kwa mujibu wa katiba ya Tanzania.
Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa kuwa Rais wa awamu ya sita, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alisema haya:-
"Nitumie fursa hii kutoa salamu za rambirambi kwa mama Janeth Magufuli, mama Suzan Magufuli, watoto wake, tunaomba Mungu awape subira katika kipindi hiki kigumu nasi tutaendelea kuwashika mkono"
" Hayati Rais Magufuli amenifundisha mengi na amenilea na kuniandaa vya kutosha, tumepoteza kiongozi shupavu. Alikua chachu ya mabadiliko"
"Leo nimekula kiapo cha juu sana nikiwa na majonzi tele na kukiwa na simanzi kubwa mtaniwia radhi nitaongea kwa uchache sana mengine tutazungumza wakati mwingine".
"Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama Taifa, kufarijiana kuonyesha upendo, undugu wetu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu na Utanzania wetu."
''Si wakati wa kutazama yaliyopita lakini ni wakati wa kutazama yaliyo mbele. Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu. Huu si wakati wakutazama mbele kwa mashaka bali kwa matumaini. Si wakati wa kunyosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono,"
"Tanzania ina hazina ya viongozi, niwahakikishie hakuna jambo litakaloharibika"



















Comments